KISA: malipo ni Hapa hapa Duniani





Siku moja kijana mmoja masikini ambae ni kama machinga alikuwa akiuza bidhaa nyumba baada ya nyumba kwa ajili ya kupata pesa kugharamia masomo yake.
Akiwa anaendelea na biashara zake alijihisi kuwa na njaa sana na siku hiyo biashara haikuwa nzuri kwake.
Akaamua kugonga kwenye nyumba mojawapo kuomba chakula. Hata hivyo aliishiwa na pozi baada ya kufunguliwa mlango na msichana mdogo aliyekuwa amependeza.
Kutokana na hofu baada ya kumuona yule msichana kijana akajitambulisha na akaomba maji ya kunywa badala ya chakula.
Yule msichana aliona kijana kuwa amechoka na mwenye njaa hivyo badala ya kumpa maji akamletea bilauri ya maziwa.
Kijana alikunywa taratibu na baada ya kumaliza akamuuliza yule msichana ni kiasi gani amlipe?
"Hutakiwi unilipe chochote," yule msichana alimjibu. "mama amenifundisha kwamba sio vizuri kupokea malipo pale unaposaidia mtu"
Kijana akasema, "Nakushukuru sana kutoka moyoni mwangu, Mungu akubariki"
Baada ya Howard Kelly (jina la yule kijana) kuondoka pale nyumbani kwao na yule msichana, alijisikia vizuri na kuendelea na shughuli zake za umachinga.
Miaka mingi ilipita na yule msichana aliyemsaidia yule kijana alipatwa na ugonjwa uliomdhoofisha sana. Madaktari wa hospitali ya wilaya aliyoko walishindwa kabisa kumtibu.
Hivyo wakaamua kumpeleka hospitali kubwa ya rufaa kwa matibabu zaidi mji mwingine mkubwa. Huko wangekutana na madaktari bingwa ambao wangeweza kumtibia ugonjwa alio nao.
Dr. Howard kelly aliitwa kwa ajili ya kumhudumia huyo mgonjwa. Baada ya kusikia jina na sehemu anayotoka yule mgonjwa akapatwa na taswira fulani iliyomkumbusha mbali sana.
Haraka haraka akiwa amevaa vazi lake la udaktari lililomkaa vema akaenda mpaka kwenye chumba alichokuwa amewekwa yule mgonjwa kumuona. Alimgundua mara moja baada ya kumuona tu. Ingawa alikuwa hana fahamu amelala hajitambui akipumulia mashine.
Daktari Kelly akaanza kumhudumia na akajiapia kutumia uwezo wake wa kitabibu kujaribu kuokoa maisha ya yule mgonjwa. Kuanzia siku hiyo akaanza kumpa 'special attention' yule mgonjwa.
Baada ya mihangaiko mingi ya tiba kwa yule mgonjwa hatimae alishinda ile vita na mgonjwa akapona.
Dr. Kelly akaomba ofisi ya malipo ya hospitali impatie yeye bili ya matibabu ya yule mgonjwa badala ya kuipeleka moja kwa moja kwa mgonjwa. Baada ya kupewa aliitizama na akaandika maneno fulani chini ya ile bili ya matibabu, na baada ya hapo bili ikapelekwa kwenye chumba cha yule mgonjwa.
Yule dada baada ya kupokea ile bili aliifungua huku akihofia gharama za matibabu zitakavyokua kubwa na angeweza kutumia maisha yake yote kuzilipa.
Ila mwishowe akashangazwa na maneno yaliyokuwa yameandikwa chini ya ile karatasi ya gharama za matibabu. Akaanza kusoma yale maandiahi yaliyoandikwa hivi;
"Gharama zote za matibabu zimelipwa kwa glasi moja ya maziwa uliyonisaidia kipindi kile nina njaa kali nilipokuwa kijana mdogo nikitafuta maisha, ni mimi Daktari Howard Kelly"
_______________________________________
TUNAJIFUNZA NINI?
Malipo siku zote hua ni hapa hapa duniani, ukitendea watu mabaya utalipwa hapa hapa na ukitendea watu mema malipo pia utayapata hapa hapa.
Tena nasema msichoke kutenda mema, maana kila mmoja wenu atalipwa kwa wakati wake pale msipozimia moyo!
SALA YANGU KWAKO.
Mwenyezi Mungu akubariki, akupe busara ya kuweza kuishi na kila mtu katika haki na kweli.
Akujalie maarifa na hekima ya kuweza kutambua thamani ya kila mmoja wetu.
Akuondolee hulka ya utengano wa aina yoyote ile uwe wa kidini, kiuchumi, kimaumbile na kadhalika...
Kwanini usiseme "Amen" ?
Labels:

Post a Comment

MKRdezign

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget