KISA: FITINA YA MAMLAKA NA FEDHA

YUPO mtu alikuwa anakabiliwa na umasikini wa kiwango cha juu. Kutokana na dhiki kumwandama, ilifikia wakati alitamani kufa kuliko kuendelea kuishi.
Pale alipokuwa anaishi, kulikuwa na eneo lenye msitu mkubwa ambao ndani yake linaishi zimwi lenye kula watu. Na katika historia ya msitu huo, hajawahi kupita binadamu salama, wote walioingia msituni waliliwa.



Yule mtu alikata shauri la kujiua na aliona njia rahisi ya kifo ni kuingia msituni ili akaliwe na zimwi. Basi akaingia katikati ya msitu!
Haikuwa uongo, alipokatiza katikati ya msitu, alijikuta amesimama mbele ya zimwi kubwa lenye hasira kali. Lile zimwi kabla halijamtafuna yule mtu, lilimuuliza: “Wewe binadamu, hujaambiwa kuwa huku naishi mimi zimwi nakula watu? Huogopi kuliwa?”
Yule mtu akajibu: “Taarifa zote ninazo, nami nimekuja huku niliwe nife, maana sina raha ya maisha.”
Zimwi akamuuliza: “Una tatizo gani mpaka useme huna raha ya maisha?”
Akajibu: “Umaskini, dhiki zangu zimenizidi kimo. Nimekata tamaa kwa ufukara nilionao.”
Zimwi liliposikia hivyo, lilimwangalia yule mtu kwa dakika kadhaa, halafu likamwambia: “Nisubiri hapohapo nakuja, usijaribu kunyanyua mguu wako hata mara moja.”
Zimwi likatoweka, baada ya muda mfupi, lilirejea likiwa limeshika vipande viwili vya miche ya dhahabu. Likamkabidhi na kumwambia yule mtu: “Umesema shida yako ni umaskini, sasa chukua hizo za dhahabu zikawe utajiri wako, ila siku ukirudi tena nakutafuna bila kukuuliza.”
Yule mtu akaondoka msituni akiwa haamini macho yake. “Bahati iliyoje, unaenda msituni na kukutana na zimwi ili likutafune ufe, lenyewe linakupa dhahabu za kubadilisha maisha yako,” alijisemea yule mtu akitembea kwa hatua za haraka kuelekea nyumbani kwake.
Alipofika nyumbani kwake, ile anafungua mlango, akamkuta malaika mtoa roho yupo ndani anamsubiri. Akamuuliza: “Umefuata nini nyumbani kwangu?”
Malaika mtoa roho akamjibu: “Mimi mgeni wako, nimefuata roho yako. Siku zako za kuishi hapa duniani zimekwisha.”
Yule mtu akalalamika: “Mbona mimi sina bahati? Yaani nimehangaika siku zote na umaskini wangu, leo nimepata dhahabu za kunifaa ili niondokane na dhiki, ndiyo siku zangu za kuishi zinafika ukingoni.”
Hata hivyo, yule mtu akamuomba malaika mtoa roho: “Naomba japo siku mbili, niuze hizi dhahabu, nipate pesa ili niwagawie maskini wenzangu angalau wabaki na nafuu ya maisha, umaskini unatesa sana. Nitajiskia vibaya nikifa na kuacha hizi dhahabu humu ndani, halafu zije ziokotwe na tajiri, wakati maskini wanateseka.”
Aliposema maneno hayo, malaika mtoa roho alimwambia: “Umeongea jambo jema lenye kumpendeza Mungu. Sadaka ni kitu kizuri sana. Basi nakupa hizo siku mbili.”
Malaika mtoa roho akaondoka zake. Yule mtu akafanya kama alivyoahidi, aliuza zile dhahabu na kupata mamilioni ya pesa. Akawazungukia maskini wale wenye dhiki na uhitaji mkubwa, aliwagawia fedha zote.
Baada ya siku mbili, yule mtu alibaki nyumbani kumsubiri malaika mtoa roho atokee. Kweli, muda ulipofika malaika alitokea. Yule mtu akatabasamu, akamuuliza: “Kabla hujanitoa roho,
ningependa kujua, je, Mungu amependa sadaka niliyotoa?”
Malaika mtoa roho akamjibu: “Mungu amefurahi sana, umewasaidia watu maskini sana kubadili maisha yao. Na kwa furaha hiyo, Mungu amekuongezea siku za kuishi. Amekupa miaka mingine 80, utakuwepo duniani na utapata mafanikio makubwa.”
Yule mtu akalalamika: “Hapana, usiniache, naomba uchukue roho yangu. Mimi sikubali kabisa, nitaishi vipi na umaskini huu? Umeniacha nimegawa mali zote ndipo unasema nitaendelea kuishi. Sasa nawezaje kuishi na ufukara huu ambao nilishaukatia tamaa?”
Malaika mtoa roho wala hakujishughulisha kumjibu, alipaa zake. Yule mtu aliwaza, akasema hawezi kuishi, akaamua kurudi msituni ili aliwe na zimwi ambalo alipoliona tu, alijigalagaza miguuni mwake huku akilia: “Nitafune nife, mimi sitaki kuishi.”
Zimwi likamuuliza: “Niambie kwanza kilichokufanya uje hapa kwa mara nyingine, nilikupa dhahabu na nikakwambia usirudi tena.”
Yule mtu alimsimulia zimwi kila kitu. Zimwi likaondoka tena, likampa miche miwili mingine ya dhahabu. Likasema: “Hii ni mara ya mwisho, usirudi tena. Ukirudi sikuulizi kitu, nakutafuna moja kwa moja.”
Alipokea miche ile ya dhahabu kwa wasiwasi, alipokuwa anatoka msituni, aliamini akifika nyumbani angekutana na malaika mtoa roho. Alifungua mlango kwa tahadhari, hakumkuta.
Alikaa kuona kama angetokea lakini haikuwa hivyo. Asubuhi ya siku iliyofuata alikwenda kuuza zile dhahabu, akapata fedha nyingi. Alifungua miradi mbalimbali ambayo ilimpa faida kubwa. Akawa tajiri mkubwa
Siku zote aliishi vizuri na watu. Aliukumbuka umaskini wake wa zamani, akawa mtoa sadaka mzuri kwa maskini. Alifanya ibada akikumbuka ahadi ya miaka 80.
Miaka 80 ilipowadia, malaika mtoa roho alimtokea na kutimiza ahadi. Roho ya mtu mwema ilitoka taratibu, huku malaika mtoa roho akimbembeleza na kumliwaza.
KISA KINGINE
Yupo mtu alikuwa maskini lakini mchamungu mno. Akawa pia mlemavu wa mguu, alitembelea gogo.
Alifanya ibada kwa uaminifu lakini shida zilimwandama, akaona bora ajiue. Alikwenda kwenye mlima mrefu wenye miamba. Akapanda mpaka kileleni, akakusudia kujitupa aangukie kwenye miamba ya chini afe.
Alipoanza kuhesabu ili ajirushe, akaona kiumbe mwenye umbo la binadamu, aliyekuwa na mavazi meupe halafu ana mbawa. Akamtolea macho yule kiumbe alipokuwa anamkaribia.
Kiumbe huyo alipomfikia yule mtu, alimwambia: “Kujiua ni dhambi mbaya mno, ukifa hapa unakwenda moja kwa moja motoni. Mwenye jukumu la kutoa roho ni mimi hapa malaika mtoa roho,”
Malaika mtoa roho alimbeba yule mtu mpaka chini, akamwambia: “Mungu amenituma nije nikuokoe kwa sababu wewe ni mtu mwema. Unafanya sana ibada ndiyo maana hakutaka ufe kifo haramu cha kujiua.”
Akaendelea kumwabia: “Najua shida yako ni umaskini, nitakupa njia nzuri. Kuna mfalme tajiri sana anauguza mwanaye kwa miaka mingi, waganga wote wameshindwa kumtibu. Na ameshatangaza kuwa siku akipatikana mtu wa kumtibu atampa nusu ya utajiri wake wote.”
Baada ya kusema hivyo, malaika mtoa roho alimchukua yule mtu mpaka kwenye mti, akamwambia achume jani. Akambeba tena na kumtua nje ya jumba la mfalme, akamwelekeza aingie ndani, aseme anayo dawa ya kumtibu mtoto wa mfalme.
Kabla ya kuondoka, malaika mtoa roho alimwambia yule maskini mlemavu: “Utapata utajiri, utaishi miaka 40 tu. Kumbuka njia zitakazompendeza Mungu na faida yako ya kesho.”
Maskini aliingia ndani, akajitambulisha. Aliporuhusiwa kumtibu mtoto wa mfalme, alilitoa jani lake, akalifikicha kisha ule unyevunyevu aliutumia kumpaka kichwani. Ghafla mgonjwa akapiga chafya, akanyanyuka. Furaha isiyo na kifani ikachukua nafasi kwenye nyumba ya mfalme.
Ahadi ilitimizwa, yule maskini alipewa nusu ya utajiri wa mfalme, akawa siyo tena maskini, akageuka tajiri mkubwa.
Kilichofuata baada ya hapo ikawa starehe, dharau, dhuluma na visa vingi. Aliutumia utajiri wake kunyanyasa wengine, kuchukua wake za watu na vurugu nyingine za kiulimwengu. Alisahau kuwa alipewa miaka 40.
Siku moja alikuwa kwenye msafara mkubwa na wapambe wake, akiwa na fedha nyingi akipeleka benki. Kuna sehemu walifika wakamkuta babu mchovu amejilaza barabarani.
Tajiri aliyekuwa maskini akapaza sauti: “Wewe maskini unalala njiani unazuia msafara wa mtu mkubwa na tajiri kama mimi, unatafuta nini? Hebu pisha njia haraka.”
Yule babu mchovu akaomba kuzungumza na tajiri, alisema analo neno muhimu kwa ajili yake. Tajiri alimfuata akiwa na hasira kali: “Wewe nani mpaka utake kuzungumza na mimi?”
Babu mchovu akamwambia: “Usiwe mkali, tuliza munkari. Unakumbuka kuna siku ulitaka kujiua na ukaokolewa na kiumbe fulani? Unakumbuka alikupa njia za kupata utajiri na alikueleza utaishi miaka 40 duniani?”
Tajiri akapigwa butwaa, akashangaa babu yule amezipataje zile habari? Babu akamuuliza tena: “Unakumbuka?”
Ikabidi tajiri ajibu kuwa anakumbuka. Alipokiri tu kuwa anakumbuka, hapohapo babu alibadilika na kugeuka yuleyule kiumbe mwenye mbawa! Malaika mtoa roho, akawambia: “Miaka 40 niliyokupa, mwisho ni leo.”
Tajiri aliyekuwa maskini akaishiwa nguvu, kwa kuchanganyikiwa akasema: “Basi naomba nafasi kidogo nipeleke hizi pesa benki.”
Malaika mtoa roho akajibu: “Kweli mali zinapendwa ila ni fitina kubwa kati ya Mungu na binadamu. Yaani badala hata kuomba nafasi usali utubu, wewe unataka kwenda benki kwanza. Nafasi hiyo huna.”
Aliposema hivyo, hapohapo malaika mtoa roho alichukua nafsi ya maskini aliyegeuka tajiri, mchezo wa duniani ukafika tamati palepale barabarani.
FITINA YA MAMLAKA NA FEDHA
Kila binadamu anapenda fedha, awe na mali nyingi. Watu wengi wanataka madaraka. Wengi ambao wamejikuta matajiri walikuwa mafukara. Idadi kubwa ya wenye mamlaka hivi sasa walikuwa watu duni nyakati zilizopita.
Fedha na mamlaka ni vitu ambavyo huwafitinisha sana binadamu na Mungu wao. Lakini ni vitu pendwa mno kwa binadamu.
Yupo mwenye fedha hutaka kufanya chochote kisa anazo fedha. Anaweza kuwaonea wengine kwa kiburi cha kwamba yeye ni tajiri.
Kuna mwenye mamlaka anaweza kufanya dhuluma na uchafuzi, hata kuua watu kwa kiburi tu cha mamlaka. Wenye fedha na mamlaka, hutenda maovu na kusahau kuwa juu yupo Mungu.
Wapo ambao hutaka wanyenyekewe hata na wazazi wao, kisa ni matajiri au wana vyeo. Wengine hutamani walambwe miguu.
USHAURI: Ukiwa tajiri au kupata madaraka, omba sana Mungu akuongoze vizuri. Hiyo ni fitina kubwa.
Ikiwa ndugu yako ni tajiri au ana madaraka makubwa, muombee sana kwa Mungu. Huo ni uadui kati yake na Mungu.
Ishi vizuri na uwe mtu mzuri kila siku, Mungu atakusimamia. Najua unapenda fedha na ungependa uwe na mamlaka, ila tambua hilo ni tego la imani. Ukipata kimojawapo au vyote kwa pamoja,
jitahidi kukaa kwenye njia ya Mungu ili ulishinde tego
Labels:

Post a Comment

MKRdezign

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget