May 2016




Kijana mmoja alishikwa akiwa anakatisha katikati
ya shamba la mzee mmoja aliyekuwa tajiri na
katili wa kutupwa katika kijiji chake na kisha
kutupwa katika shimo lenye urefu wa zaidi ya futi
40.
Akiwa mle ndani alilia sana tena kwa uchungu na
hakuwa na jinsi kwani mle ndani kulikuwa na
baadhi ya mizoga na mabaki ya baadhi ya viumbe
vilivyotupwa mle na kufa kwa kushindwa kujiokoa
kutoka katika shimo lile kuwa refu.
Akafikiri namna ya kujitoa pale na kuanza
kujirusha ili ajitoe mle ndani lakini kila alipozidi
kuruka ndio jinsi misuli yake ilivyozidi kuwa dhaifu
na dhaifu zaidi.
Mwishowe akafikiri aache kwani angepoteza nguvu
zake na mwisho kufa hivyo ni nafuu abaki bila ya
kufanya chochote na kusubiri muda wa kufa
ufike.
Akiwa ameshaamua kusubiri kifo, mara akasikia
sauti kutoka upande wa pili ambako kuna mtu
alisikika akipiga kelele za kuomba msaada wa
kujinasua na shimo lake lilikuwa chini zaidi kwa
futi 10...uuuuh akavuta pumzi na kuona kumbe
wako wengi wanaohitaji msaada mle ndani.
Akakaa kimya na kusikia jitihada za mtu yule
akijitahidi kujinasua na mchanga ukimwagika
chini... Ghafla akajawa na nguvu na hamasa ya
kutoka mle ndani akasimama na kuanza kujinasua
hatua moja baada ya nyingine na hatimaye
akafanikiwa kujinasua mle ndani na kuondoka
kwenda kwake.
Funzo
Yale maumivu ya mapito magumu unayofikiri
unayapitia peke yako, kumbuka kuna watu
wanaumia zaidi yako
Kila siku jipe maneno yenye matumaini na amini
katika kila changamoto unatakiwa kuwa mvumilivu
huku ukitafuta njia ya kujinasua
Kila maumivu ambayo yanakujia usiyape muda
wa kukaa ndani yako zaidi ya kuyapa kisogo
yapotee kwani kwa kila giza la leo kumbuka
asubuhi inakuja na nuru itatokea
Jipe ujasiri mwenyewe , chukua kioo jiangalie na
kusema " mimi ni zaidi ya kila kitu na nitafanikiwa
kwa kila jambo na kumwomba Mungu akutangulie
na kuwa mlinzi wako"
Kila mara jaribu kuyakazia uso matatizo yaliyo
mbele yako na kuhakikisha unayatatua na
kuyageuza kuwa fursa kwani hakuna kizuri
kinachokuja kirahisi rahisi labda kutoka kwa
kameruni
Baba Mungu, namwombea kijana huyu
anayesoma ujumbe huu umpe imani, nguvu na
ujasiri wa kuyahimili matatizo yake na kumfanya
aje kuwa mtu mwenye mafanikio ..AMEN

Binti wa miaka 19 ambaye aliacha shule baada ya baba na mama kufa katika ajali mbaya na ndugu kutompa msaada aliamua kuondoka nyumbani na kwenda kuishi na kijana mmoja. Miaka 10 sasa amekuwa anakaa na rafiki yake wa kiume avutaye bangi katika ghetto.
Amekuwa anapewa fedha kidogo kutoka kwa huyo mpenzi wake ili anunulie chakula na kula na marafiki wa kaka huyo baada ya kutumika kimapenzi kwa wiki zima huku akiuza maji ya kunywa.
Baada ya muda akajikuta ni mjamzito na huyo kijana akamwambia watoe tu mimba hiyo.Akampa fedha kidogo na kumwambia aongeze nyingine ambazo amekuwa akimpa ili akatoe mimba bila kukumbuka kuwa fedha hizo zimekuwa zikitumika kwa ajili ya chakula.
Siku ya pili yake akiwa anatoka chumbani mwao kwenda kutoa mimba, akpita kwenye korido ambako akakanyanga sakafu ambayo ina maji na kuteleza. yule kijana akamwona wakati anaangukia tumbo pale sakafuni na akasema, “ amini au usiamini hii ndio njia rahisi niliyoitaka uitumie kutoa mimba hiyo”
Kijana akamchukua binti wakati huo damu nyingi zikimtoka na kumwambia aende bafuni akanawe.Lakini kwa nguvu za mwenyezi Mungu yule dada alipona ingawa mimba ilitoka na akaumwa kwa zaidi ya wiki bila msaada wowote ule..
Siku moja akiwa anauza maji akakutana na muuza magazeti na kumpa maji pakiti moja bure na kumwambia, “leo ni miaka kumi tangu baba na mama yangu wafariki katika ajali mbaya, hivyo sitajali mchumba wangu atasemaje au kunifanya nini kwa kutoa maji haya bure, ila mimi nitatoa maji bure kama kumbukumbu ya siku hii yenye simanzi kwangu”.
Akiwa anataka kuondoka yule muuza magazeti akamwambia kuwa kuna nafasi ya kazi sehemu na kuwa atamsaidia kuandika barua ya kuomba. Yule dada ailishukuru na akawa anampigia mara kwa mara yule muuza magazeti mpaka siku akaitwa kwenda kwenye usaili.
Siku ya usaili akiwa njiani anaelekea huko akakutana na mama mmoja akiwa na gari aina ya BMW likiwa nimeishiwa mafuta. Yule dada akamuuliza mama, Je unahitaji msaada gani?
yule mama akamwambia nimeishiwa mafuta na sijui cha kufanya hapa. Dada akachukua kidumu na kwenda mbio kumnunulia mafuta yule mama na akarudi na kumpa.
Yule mama alipotaka kumpa hela, dada akakataa akasema nimekuona nikamkumbuka mama yangu hivyo nimefurahi kukusaidia, kama hutajali naomba niwahi sehemu.
Kufika kwenye usaili dada akashangaa kuona kumbe yule mama mwenye BMW ndio boss wa ile kampuni na akafanyiwa usahili na kuanza kazi na sasa anajimudu kifedha na ana biashara zake.
Na sasa hakai tena na yule kijana mvuta bangi wakati nusu ya utajiri wake anaupeleka kwenye vituo vya kulelea watoto yatima.
Nami leo nakuombea unayeisoma habari hii, Mungu akujalie na kukufungulia milango ya mafanikio katika kila jaribu unalolipitia na ukumbuke kuwasaidia wanao hitaji msaada wako.
Comment neno “Amen” na kisha share



Dada alikuwa airport akisubiri connetion ya ndege yake, wakatangaziwa ni 2 hrs waiting time.
Akaamua kununua gazeti na box Dogo la biscuits, akatafuta sehemu akakaa kusoma gazeti kusubiri muda ufike wa kuingia kwenye ndege, alipokaa pembeni yake kulikuwa na kaka nae anasoma gazeti akisubiri ndege. Dada alishangaa alipokuwa akitoa biscuit kwenye box aliloliweka pembeni yule kaka nae anachukua moja anakula, akamwangalia kwa hasira, kaka akawa anatabasamu.
Dada akakasirika akataka kumtolea maneno machafu akajizuia. Ukawa mchezo kila dada akichomoa biscuit moja yule kaka nae anachukua moja. Ikaendelea hadi ikabakia biscuit moja. Yule kaka akawahi kuichukua akaimega nusu akampa yule dada, ...dada kwa ghadhabu akanyanyuka akamtukana sana yule kaka na maneno ya kumdhalilisha kwanini anavamia vitu vya watu asinunue vyake!! Kaka alikaa kimya bila kumjibu yule dada.
Mara wakatangaziwa muda wa kuingia kwenye ndege, yule dada akaingia akimuacha kaka nae akisubiri ndege yake. Alipokaa kwenye siti yake akafungua mkoba aweke simu yake, mara alishtuka kuona box lake la biscuits zima wala halijafunguliwa, kumbe alikuwa anakula biscuits za yule kaka. Akajutia sana akatokwa na machoz jinsi alivyomdhalilisha yule kaka, na muda wa kurudi kuomba msamaha haupo tena kwani milango ya ndege ilishafungwa na kuanza kuondoka. "Muda wa kuomba msamaha kwa uliyemkosea upo usisubiri milango ifungwe"... Kiburi ni sifa ya Shetani

YUPO mtu alikuwa anakabiliwa na umasikini wa kiwango cha juu. Kutokana na dhiki kumwandama, ilifikia wakati alitamani kufa kuliko kuendelea kuishi.
Pale alipokuwa anaishi, kulikuwa na eneo lenye msitu mkubwa ambao ndani yake linaishi zimwi lenye kula watu. Na katika historia ya msitu huo, hajawahi kupita binadamu salama, wote walioingia msituni waliliwa.



Yule mtu alikata shauri la kujiua na aliona njia rahisi ya kifo ni kuingia msituni ili akaliwe na zimwi. Basi akaingia katikati ya msitu!
Haikuwa uongo, alipokatiza katikati ya msitu, alijikuta amesimama mbele ya zimwi kubwa lenye hasira kali. Lile zimwi kabla halijamtafuna yule mtu, lilimuuliza: “Wewe binadamu, hujaambiwa kuwa huku naishi mimi zimwi nakula watu? Huogopi kuliwa?”
Yule mtu akajibu: “Taarifa zote ninazo, nami nimekuja huku niliwe nife, maana sina raha ya maisha.”
Zimwi akamuuliza: “Una tatizo gani mpaka useme huna raha ya maisha?”
Akajibu: “Umaskini, dhiki zangu zimenizidi kimo. Nimekata tamaa kwa ufukara nilionao.”
Zimwi liliposikia hivyo, lilimwangalia yule mtu kwa dakika kadhaa, halafu likamwambia: “Nisubiri hapohapo nakuja, usijaribu kunyanyua mguu wako hata mara moja.”
Zimwi likatoweka, baada ya muda mfupi, lilirejea likiwa limeshika vipande viwili vya miche ya dhahabu. Likamkabidhi na kumwambia yule mtu: “Umesema shida yako ni umaskini, sasa chukua hizo za dhahabu zikawe utajiri wako, ila siku ukirudi tena nakutafuna bila kukuuliza.”
Yule mtu akaondoka msituni akiwa haamini macho yake. “Bahati iliyoje, unaenda msituni na kukutana na zimwi ili likutafune ufe, lenyewe linakupa dhahabu za kubadilisha maisha yako,” alijisemea yule mtu akitembea kwa hatua za haraka kuelekea nyumbani kwake.
Alipofika nyumbani kwake, ile anafungua mlango, akamkuta malaika mtoa roho yupo ndani anamsubiri. Akamuuliza: “Umefuata nini nyumbani kwangu?”
Malaika mtoa roho akamjibu: “Mimi mgeni wako, nimefuata roho yako. Siku zako za kuishi hapa duniani zimekwisha.”
Yule mtu akalalamika: “Mbona mimi sina bahati? Yaani nimehangaika siku zote na umaskini wangu, leo nimepata dhahabu za kunifaa ili niondokane na dhiki, ndiyo siku zangu za kuishi zinafika ukingoni.”
Hata hivyo, yule mtu akamuomba malaika mtoa roho: “Naomba japo siku mbili, niuze hizi dhahabu, nipate pesa ili niwagawie maskini wenzangu angalau wabaki na nafuu ya maisha, umaskini unatesa sana. Nitajiskia vibaya nikifa na kuacha hizi dhahabu humu ndani, halafu zije ziokotwe na tajiri, wakati maskini wanateseka.”
Aliposema maneno hayo, malaika mtoa roho alimwambia: “Umeongea jambo jema lenye kumpendeza Mungu. Sadaka ni kitu kizuri sana. Basi nakupa hizo siku mbili.”
Malaika mtoa roho akaondoka zake. Yule mtu akafanya kama alivyoahidi, aliuza zile dhahabu na kupata mamilioni ya pesa. Akawazungukia maskini wale wenye dhiki na uhitaji mkubwa, aliwagawia fedha zote.
Baada ya siku mbili, yule mtu alibaki nyumbani kumsubiri malaika mtoa roho atokee. Kweli, muda ulipofika malaika alitokea. Yule mtu akatabasamu, akamuuliza: “Kabla hujanitoa roho,
ningependa kujua, je, Mungu amependa sadaka niliyotoa?”
Malaika mtoa roho akamjibu: “Mungu amefurahi sana, umewasaidia watu maskini sana kubadili maisha yao. Na kwa furaha hiyo, Mungu amekuongezea siku za kuishi. Amekupa miaka mingine 80, utakuwepo duniani na utapata mafanikio makubwa.”
Yule mtu akalalamika: “Hapana, usiniache, naomba uchukue roho yangu. Mimi sikubali kabisa, nitaishi vipi na umaskini huu? Umeniacha nimegawa mali zote ndipo unasema nitaendelea kuishi. Sasa nawezaje kuishi na ufukara huu ambao nilishaukatia tamaa?”
Malaika mtoa roho wala hakujishughulisha kumjibu, alipaa zake. Yule mtu aliwaza, akasema hawezi kuishi, akaamua kurudi msituni ili aliwe na zimwi ambalo alipoliona tu, alijigalagaza miguuni mwake huku akilia: “Nitafune nife, mimi sitaki kuishi.”
Zimwi likamuuliza: “Niambie kwanza kilichokufanya uje hapa kwa mara nyingine, nilikupa dhahabu na nikakwambia usirudi tena.”
Yule mtu alimsimulia zimwi kila kitu. Zimwi likaondoka tena, likampa miche miwili mingine ya dhahabu. Likasema: “Hii ni mara ya mwisho, usirudi tena. Ukirudi sikuulizi kitu, nakutafuna moja kwa moja.”
Alipokea miche ile ya dhahabu kwa wasiwasi, alipokuwa anatoka msituni, aliamini akifika nyumbani angekutana na malaika mtoa roho. Alifungua mlango kwa tahadhari, hakumkuta.
Alikaa kuona kama angetokea lakini haikuwa hivyo. Asubuhi ya siku iliyofuata alikwenda kuuza zile dhahabu, akapata fedha nyingi. Alifungua miradi mbalimbali ambayo ilimpa faida kubwa. Akawa tajiri mkubwa
Siku zote aliishi vizuri na watu. Aliukumbuka umaskini wake wa zamani, akawa mtoa sadaka mzuri kwa maskini. Alifanya ibada akikumbuka ahadi ya miaka 80.
Miaka 80 ilipowadia, malaika mtoa roho alimtokea na kutimiza ahadi. Roho ya mtu mwema ilitoka taratibu, huku malaika mtoa roho akimbembeleza na kumliwaza.
KISA KINGINE
Yupo mtu alikuwa maskini lakini mchamungu mno. Akawa pia mlemavu wa mguu, alitembelea gogo.
Alifanya ibada kwa uaminifu lakini shida zilimwandama, akaona bora ajiue. Alikwenda kwenye mlima mrefu wenye miamba. Akapanda mpaka kileleni, akakusudia kujitupa aangukie kwenye miamba ya chini afe.
Alipoanza kuhesabu ili ajirushe, akaona kiumbe mwenye umbo la binadamu, aliyekuwa na mavazi meupe halafu ana mbawa. Akamtolea macho yule kiumbe alipokuwa anamkaribia.
Kiumbe huyo alipomfikia yule mtu, alimwambia: “Kujiua ni dhambi mbaya mno, ukifa hapa unakwenda moja kwa moja motoni. Mwenye jukumu la kutoa roho ni mimi hapa malaika mtoa roho,”
Malaika mtoa roho alimbeba yule mtu mpaka chini, akamwambia: “Mungu amenituma nije nikuokoe kwa sababu wewe ni mtu mwema. Unafanya sana ibada ndiyo maana hakutaka ufe kifo haramu cha kujiua.”
Akaendelea kumwabia: “Najua shida yako ni umaskini, nitakupa njia nzuri. Kuna mfalme tajiri sana anauguza mwanaye kwa miaka mingi, waganga wote wameshindwa kumtibu. Na ameshatangaza kuwa siku akipatikana mtu wa kumtibu atampa nusu ya utajiri wake wote.”
Baada ya kusema hivyo, malaika mtoa roho alimchukua yule mtu mpaka kwenye mti, akamwambia achume jani. Akambeba tena na kumtua nje ya jumba la mfalme, akamwelekeza aingie ndani, aseme anayo dawa ya kumtibu mtoto wa mfalme.
Kabla ya kuondoka, malaika mtoa roho alimwambia yule maskini mlemavu: “Utapata utajiri, utaishi miaka 40 tu. Kumbuka njia zitakazompendeza Mungu na faida yako ya kesho.”
Maskini aliingia ndani, akajitambulisha. Aliporuhusiwa kumtibu mtoto wa mfalme, alilitoa jani lake, akalifikicha kisha ule unyevunyevu aliutumia kumpaka kichwani. Ghafla mgonjwa akapiga chafya, akanyanyuka. Furaha isiyo na kifani ikachukua nafasi kwenye nyumba ya mfalme.
Ahadi ilitimizwa, yule maskini alipewa nusu ya utajiri wa mfalme, akawa siyo tena maskini, akageuka tajiri mkubwa.
Kilichofuata baada ya hapo ikawa starehe, dharau, dhuluma na visa vingi. Aliutumia utajiri wake kunyanyasa wengine, kuchukua wake za watu na vurugu nyingine za kiulimwengu. Alisahau kuwa alipewa miaka 40.
Siku moja alikuwa kwenye msafara mkubwa na wapambe wake, akiwa na fedha nyingi akipeleka benki. Kuna sehemu walifika wakamkuta babu mchovu amejilaza barabarani.
Tajiri aliyekuwa maskini akapaza sauti: “Wewe maskini unalala njiani unazuia msafara wa mtu mkubwa na tajiri kama mimi, unatafuta nini? Hebu pisha njia haraka.”
Yule babu mchovu akaomba kuzungumza na tajiri, alisema analo neno muhimu kwa ajili yake. Tajiri alimfuata akiwa na hasira kali: “Wewe nani mpaka utake kuzungumza na mimi?”
Babu mchovu akamwambia: “Usiwe mkali, tuliza munkari. Unakumbuka kuna siku ulitaka kujiua na ukaokolewa na kiumbe fulani? Unakumbuka alikupa njia za kupata utajiri na alikueleza utaishi miaka 40 duniani?”
Tajiri akapigwa butwaa, akashangaa babu yule amezipataje zile habari? Babu akamuuliza tena: “Unakumbuka?”
Ikabidi tajiri ajibu kuwa anakumbuka. Alipokiri tu kuwa anakumbuka, hapohapo babu alibadilika na kugeuka yuleyule kiumbe mwenye mbawa! Malaika mtoa roho, akawambia: “Miaka 40 niliyokupa, mwisho ni leo.”
Tajiri aliyekuwa maskini akaishiwa nguvu, kwa kuchanganyikiwa akasema: “Basi naomba nafasi kidogo nipeleke hizi pesa benki.”
Malaika mtoa roho akajibu: “Kweli mali zinapendwa ila ni fitina kubwa kati ya Mungu na binadamu. Yaani badala hata kuomba nafasi usali utubu, wewe unataka kwenda benki kwanza. Nafasi hiyo huna.”
Aliposema hivyo, hapohapo malaika mtoa roho alichukua nafsi ya maskini aliyegeuka tajiri, mchezo wa duniani ukafika tamati palepale barabarani.
FITINA YA MAMLAKA NA FEDHA
Kila binadamu anapenda fedha, awe na mali nyingi. Watu wengi wanataka madaraka. Wengi ambao wamejikuta matajiri walikuwa mafukara. Idadi kubwa ya wenye mamlaka hivi sasa walikuwa watu duni nyakati zilizopita.
Fedha na mamlaka ni vitu ambavyo huwafitinisha sana binadamu na Mungu wao. Lakini ni vitu pendwa mno kwa binadamu.
Yupo mwenye fedha hutaka kufanya chochote kisa anazo fedha. Anaweza kuwaonea wengine kwa kiburi cha kwamba yeye ni tajiri.
Kuna mwenye mamlaka anaweza kufanya dhuluma na uchafuzi, hata kuua watu kwa kiburi tu cha mamlaka. Wenye fedha na mamlaka, hutenda maovu na kusahau kuwa juu yupo Mungu.
Wapo ambao hutaka wanyenyekewe hata na wazazi wao, kisa ni matajiri au wana vyeo. Wengine hutamani walambwe miguu.
USHAURI: Ukiwa tajiri au kupata madaraka, omba sana Mungu akuongoze vizuri. Hiyo ni fitina kubwa.
Ikiwa ndugu yako ni tajiri au ana madaraka makubwa, muombee sana kwa Mungu. Huo ni uadui kati yake na Mungu.
Ishi vizuri na uwe mtu mzuri kila siku, Mungu atakusimamia. Najua unapenda fedha na ungependa uwe na mamlaka, ila tambua hilo ni tego la imani. Ukipata kimojawapo au vyote kwa pamoja,
jitahidi kukaa kwenye njia ya Mungu ili ulishinde tego





Siku moja kijana mmoja masikini ambae ni kama machinga alikuwa akiuza bidhaa nyumba baada ya nyumba kwa ajili ya kupata pesa kugharamia masomo yake.
Akiwa anaendelea na biashara zake alijihisi kuwa na njaa sana na siku hiyo biashara haikuwa nzuri kwake.
Akaamua kugonga kwenye nyumba mojawapo kuomba chakula. Hata hivyo aliishiwa na pozi baada ya kufunguliwa mlango na msichana mdogo aliyekuwa amependeza.
Kutokana na hofu baada ya kumuona yule msichana kijana akajitambulisha na akaomba maji ya kunywa badala ya chakula.
Yule msichana aliona kijana kuwa amechoka na mwenye njaa hivyo badala ya kumpa maji akamletea bilauri ya maziwa.
Kijana alikunywa taratibu na baada ya kumaliza akamuuliza yule msichana ni kiasi gani amlipe?
"Hutakiwi unilipe chochote," yule msichana alimjibu. "mama amenifundisha kwamba sio vizuri kupokea malipo pale unaposaidia mtu"
Kijana akasema, "Nakushukuru sana kutoka moyoni mwangu, Mungu akubariki"
Baada ya Howard Kelly (jina la yule kijana) kuondoka pale nyumbani kwao na yule msichana, alijisikia vizuri na kuendelea na shughuli zake za umachinga.
Miaka mingi ilipita na yule msichana aliyemsaidia yule kijana alipatwa na ugonjwa uliomdhoofisha sana. Madaktari wa hospitali ya wilaya aliyoko walishindwa kabisa kumtibu.
Hivyo wakaamua kumpeleka hospitali kubwa ya rufaa kwa matibabu zaidi mji mwingine mkubwa. Huko wangekutana na madaktari bingwa ambao wangeweza kumtibia ugonjwa alio nao.
Dr. Howard kelly aliitwa kwa ajili ya kumhudumia huyo mgonjwa. Baada ya kusikia jina na sehemu anayotoka yule mgonjwa akapatwa na taswira fulani iliyomkumbusha mbali sana.
Haraka haraka akiwa amevaa vazi lake la udaktari lililomkaa vema akaenda mpaka kwenye chumba alichokuwa amewekwa yule mgonjwa kumuona. Alimgundua mara moja baada ya kumuona tu. Ingawa alikuwa hana fahamu amelala hajitambui akipumulia mashine.
Daktari Kelly akaanza kumhudumia na akajiapia kutumia uwezo wake wa kitabibu kujaribu kuokoa maisha ya yule mgonjwa. Kuanzia siku hiyo akaanza kumpa 'special attention' yule mgonjwa.
Baada ya mihangaiko mingi ya tiba kwa yule mgonjwa hatimae alishinda ile vita na mgonjwa akapona.
Dr. Kelly akaomba ofisi ya malipo ya hospitali impatie yeye bili ya matibabu ya yule mgonjwa badala ya kuipeleka moja kwa moja kwa mgonjwa. Baada ya kupewa aliitizama na akaandika maneno fulani chini ya ile bili ya matibabu, na baada ya hapo bili ikapelekwa kwenye chumba cha yule mgonjwa.
Yule dada baada ya kupokea ile bili aliifungua huku akihofia gharama za matibabu zitakavyokua kubwa na angeweza kutumia maisha yake yote kuzilipa.
Ila mwishowe akashangazwa na maneno yaliyokuwa yameandikwa chini ya ile karatasi ya gharama za matibabu. Akaanza kusoma yale maandiahi yaliyoandikwa hivi;
"Gharama zote za matibabu zimelipwa kwa glasi moja ya maziwa uliyonisaidia kipindi kile nina njaa kali nilipokuwa kijana mdogo nikitafuta maisha, ni mimi Daktari Howard Kelly"
_______________________________________
TUNAJIFUNZA NINI?
Malipo siku zote hua ni hapa hapa duniani, ukitendea watu mabaya utalipwa hapa hapa na ukitendea watu mema malipo pia utayapata hapa hapa.
Tena nasema msichoke kutenda mema, maana kila mmoja wenu atalipwa kwa wakati wake pale msipozimia moyo!
SALA YANGU KWAKO.
Mwenyezi Mungu akubariki, akupe busara ya kuweza kuishi na kila mtu katika haki na kweli.
Akujalie maarifa na hekima ya kuweza kutambua thamani ya kila mmoja wetu.
Akuondolee hulka ya utengano wa aina yoyote ile uwe wa kidini, kiuchumi, kimaumbile na kadhalika...
Kwanini usiseme "Amen" ?

Aliyoyasema Mke wake siku ya jubilei ya kutimiza miaka nane ya ndoa yao.




Mpendwa mme wangu,
Umenifanya nijivunie sana kuwa mke wako. Tunaposheherekea miaka yetu nane ya Ndoa ningependa niongee haya machache.
Pale wanawake wenzangu wanapolalamika kuhusiana na waume zao kutokuwa waaminifu katika ndoa zao, pale ambapo wanaogopa waume zao kuwaletea magonjwa ndani ya nyumba, wewe umekuwa mume muaminifu, sijawahi kukushuku lolote, uananipa utulivu wa nafsi. Ndio maana sikuchoki!
Pale ambapo wanawake wenzangu wanalalamika kuhusiana na ubabe na masumbwi ndani ya nyumba, wewe unanishangaza! Unanipetipeti kama Malkia kwanini mimi nisikupetipeti kama mfalme!? Oh Asante Mungu kwa hilo.
Pale ambapo wanawake wenzangu wamekuwa wakilalamika na kutoa siri zao za ndani ya ndoa kwenye magroup ya watsapp na vikundi vyao kwamba waume zao hawawaridhishi, wewe umekuwa wa tofauti na sioni lolote kwako linaloshahibiana na wasemayo kutoka kwa waume zao.
Pale ambapo wanawake wengine wanajuta kwanini waliolewa, wewe kila siku unanionesha kwamba kuolewa na wewe ulikuwa uamuzi wangu wa busara kabisa ambao sijawahi kuufanya kabla.
Pale ambapo wanawake wenzangu wamekuwa wakilia na kumuomba Mungu juu ya stress za ndoa zao, wewe umenipa sababu ya kumshukuru Mungu na kumpa sifa kwa kunikutanisha na wewe.
Pale ambapo wanawake wenzangu wameumizwa katika mahusiano na kupelekea kuwachukia wanaume na kuona kama ni mbwa, wewe umenifanya niheshimu wanaume na kuwa na mawazo chanya juu ya wanaume!
Pale ambapo wanawake wenzangu wamekatishwa tamaa na waume zao kukimbia majukumu ya kulea baada ya kupata ujauzito, wewe umeonesha ni jinsi gani ulivyo baba bora, usie kimbia majukumu yako.
Pale ambapo wanawake wenzangu wamejihisi kuwa wapweke ndani ya ndoa, ingawa waume zao wapo, wewe umekua bestfriend wangu, unajua jinsi ya kunifanya nicheke na kutabasamu, nakumiss muda wote ubapokuwa mbali na mimi!
Pale ambapo wanawake wenzangu hawawaamini waume zao, wewe uko muwazi kwangu, unanieleza ratiba zako, ninawajua rafiki zako, sihitaji kukuchunguza na kukubana kwa sababu sikuhisi kwa lolote, hujabadilika tolea uchumba mpaka hivi sasa.
Pale ambapo wanawake wenzangu wamekuwa wakilalamika juu ya waume zao kuchelewa kurudi nyumbani, wewe umekuwa ukiwahi na hautaki chakula cha usiku ule peke yako, unataka wote kama familia mimi, wanao tuizunguke meza na tule kwa pamoja!
Pale ambapo wanawake wenzangu wamekuwa wakilalamika usiri ndani ya ndoa, wewe umekuwa ukinishirikisha miradi ya maendeleo kwa ustawi wa familia na ninajivunia kuwa sehemu ya mafanikio ya miradi hiyo, umeniamini nikaisimamia vilivyo na inakua kila uchweo!
Ninasheherekea hilo mfalme wangu, mimi ni mke bora kwa vile ninae mume bora. Jinsi unavyonipenda inanipa uhuru wa kukupenda pia. Furaha ilioje kuwa mke wako.
Pamoja na kuwa na mapugufu ya hapa na pale, naamini yanavumilika na uzuri ni kwamba najaribu kusheherekea mapungufu yako na sitaki yatutenganishe, maana hata mimi nina mapungufu yangu na unanivumilia vilevile!
Nakupenda Baba watoto!

"Je utakubali kuolewa na mimi?"





Akamuuliza mpenzi wake ambae ni mtarajiwa wake katika ndoa.
Mwanamke akainua kinywa chake kutaka kuzungumza lakini mwanaume akamzuia na kumwambia yafuatayo;
Akamwambia kabla hujanipa jibu lako, naomba uelewe kabisa ni nini nachokimaanisha na nini haswa kipo katika mahusiano ya ndoa.
Niwe mkweli kwako;
Ninakuomba uje kuwa mke wangu wa ndoa, katika Ndoa mapenzi huwa ni daraja jingine kabisa maana huko kuna nafasi nyingi zaidi za kuonesha upendo kati yetu.
Nitakufanya kama malkia wangu, nitakupenda siku zote, na utakuwa kipaumbele changu.
Mwanaume akamshika mkono mwanamke wake na kuendelea kumwambia, "Lakini unapaswa kutambua kwamba katikati ya ndoa yetu kutakua na misuguano na mikwaruzano ya hapa na pale, mimi sio mkamilifu asilimia 100.
Ninaweza nikakuudhi mara kadhaa, ninaweza kukusababishia hasira, haijalishi ni kiasi gani nitakukosea naomba tu utambue kuwa kukusoma na kukuelewa wewe ni somo endelevu.
Mimi na wewe tumekutana ukubwani, tumelelewa katika familia tofauti. Lazima tu nitakuwa na baadhi ya vitu usivyovipenda. Nivumilie!
Ndio maana siku zote namuomba Mungu azidi kunifunza kukupenda wewe!
Mwanamke akamtizama mwanaume wake kwa macho ya upendo!
Mwanaume akaendela, "vitu vingi sana utavitarajia kwangu nikiwa kama mume wako. Nitakuwa kichwa cha nyumba, nitahitajika kutunza familia na kuiongoza vema, lakini lazima kutakuwa na siku njema na mbaya.
Katika siku mbaya, nifariji, nipe moyo, niamini mimi, nikumbatie na uwe nguzo yangu. Nitafute pale nitakapopotea, nisamehe pale nitakapokosea.
Lakini kama unaona nakuomba vitu vingi basi usikubali kuolewa na mimi. Nataka niwe mkweli kwako kabla hatujaingia katika Ndoa.
Mwanamke akamkisi mwanaume wake katika paji la uso na kumwambia yafuatayo;
"kabla sijakubali proposal yako ya kunioa naomba na mimi niwe mkweli kwako. Nakupenda na ninafahamu ni nini maana ya upendo.
Upendo hauhesabu mabaya, upendo husamehe, upendo huvumilia. Ningeweza kuwa single maisha yangu yote lakini sicho kitu ambacho nilikihitaji.
Ninachokihitaji ni wewe tu!
Nahitaji mapenzi kutoka kwako, nitakupenda hata kipindi kibaya katika maisha. Nina moyo ambao umejazwa upendo, na ninahitaji sana niutumie kwako."
Mwanamke akamtizama mwanaume wake na kuendelea kumwambia;
"Ninakupenda jinsi ulivyo, mali na fedha tutazitafuta pamoja furaha na amani niliyonayo ni mtaji tosha.
Nafurahi kwa kuwa umesema utajifunza kuishi na mimi, basi nami pia nitajifunza kuishi na wewe.
Katika ndoa, naweza nikasema mambo ya kuudhi na kufanya yale ya kuudhi, naweza nikawa sina mood muda mwingine, naweza nikawa nimechoka, na kuhitaji muda kidogo peke yangu. Hiyo haitamaanisha sikupendi tena la hasha ni darasa tu la kujifunza kuishi pamoja."
Muda mwingine naweza nikahangaika kubalance kuwa mke, mama, binti wa wazazi wangu, mfanyakazi ofisini na dada wa ndugu zangu, naomba nivumilie kwa hilo na unielewe pia."
Nipende, nijali, niheshimu, nivumilie hata pale nitakapovaa gauni la ujauzito kama Mungu akitujaalia, nami nitakupenda siku zote."
Mwanamke akafumba macho na kufungua kuendelea kuongea "itakuwa ndoto yangu imekamilika kuishi na wewe, mfalme wangu. Mwalimu wangu na mwanafunzi wangu vilevile. Sihitaji kuwa peke yangu, nahitaji kuwa na wewe.
Nahitaji kuwa mke mwema kwako.
Kwa kujiamini kabisa nakujibu Ndio nitakubali kuolewa na wewe"

NOTEBOOK YA NDOA


Baada ya kumaliza sherehe ya ndoa yao, mama wa bibi harusi alimpa binti yake notebook yenye namba mpya ya Akaunti ya benki ikiwa na kiasi cha shilingi laki tatu.
Mama alimwambia hivi, "binti yangu, chukua hii notebook, itunze kama kitu cha kuandikia rekodi katika maisha yako ya ndoa, chochote cha kufurahisha kitakachotokea katika maisha yako haya mapya na mumeo, weka pesa katika akaunti hii na uandike katika notebook juu ya hiyo furaha yako/yenu.
Matukio ya kufurahisha yatakavyotamalaki katika ndoa yenu yakizidi nawewe ndio uzidi kuweka kiwango zaidi cha fedha utakayokuwa nayo kama akiba bila kusahau kuweka rekodi ya hiyo furaha.
Fanya hili na mumeo ili mtakapotizama baada ya miaka kadhaa mtambue ni kwa kiasi gani mlikuwa na furaha katika ndoa yenu.
Binti alipokea hayo maelekeza na akaenda kumueleza na mumewe. Wanandoa waliona kwamba ni jambo jema kwao na vilevile ni njia mojawapo ya utunzaji wa fedha.
Wakawa wakisubiri tu panapofuraha kati yao ili wewekeze hizo pesa.
Hivi ndivyo ile notebook ilisomeka baada ya kipindi kirefu kidogo cha ndoa yao;
7 February- Tsh 100,000 - birthday ya kwanza ya mume wangu tukiwa katika ndoa
1 March- Tsh 110,000- Mume wangu amepandishwa cheo kazini.
20 March- Tsh 120,000 - Tumeenda likizo Zanzibar.
29 April - Tsh 125,000 - Ujauzito wa kwanza.
5 september - Tsh 130,000 Mume wangu amenifulia nguo zangu zote chafu baada ya mimi kuwa hoi ujauzito ukinisumbua.
8 October - Nimemnunulia mume wangu saa aipendayo, amefurahi sana....
List ilikuwa ndefu sana........
Hata hivyo miaka ilisonga na wanandoa wakaanza ugomvi na mabishano baina yao. Wakawa hawana ukaribu tena na kila mmoja akawa anajutia ndoa yao, hakukuwa na mapenzi tena kati yao.
Siku moja binti alimpigia mama yake simu. "mama siwezi kuvumilia tena, tumeamua tuachane, najuta kwanini nilikubali kuolewa na huyu mwanamume!" Binti alisikika na mama yake akiongea.
Mama yake akamjibu, "Mwanangu siungi mkono jambo unalotaka kufanya ila siyo kesi kubwa fanya kile ambacho moyo wako umeamua ila kabla ya hapo fanya kitu kimoja. Unakumbuka ile notebook niliyokupa? Nenda katoe pesa zote benki na utumie na mumeo kabla hamjaachana.!
Hivyo yule binti alienda benki, na wakati amesimama kwenye foleni alichukua ile notebook na kuanza kusoma matukio ya furaha na faraja waliyoyapitia yeye na mumewe.
Jinsi alivyokuwa akizidi kuyasoma yale matukio ndipo kumbukumbu za furaha na mapenzi vilizidi kuujaza moyo wake, na machozi yakiwa yanamtoka, akaghairisha na kurudi nyumbani.
Alipofika nyumbani alimkabidhi mumewe ile notebook na kumwambia aende akatoe zile pesa wagawane kabla hawajatalikiana.
Nae alipoenda benki akiwa katika foleni akisoma ile notebook nae alipatwa na hali ile ile, aliamua asitoe zile pesa. Na akarudi nyumbani.
Akiwa na mkewe, waliamua kufanya mahesabu wajue ni kiasi gani kilichokuwemo katika akaunti, walipofanya majumuisho ya matukio yote ya furaha waliyoyarekodi walijikuta wakiwa na shilingi milioni tatu na laki tano.
Kwa mshangao mume akamwambia kwamba leo ndio nimegundua ni kwa thamani gani ninakupenda, ni kwa kiasi gani umeleta furaha kwenye maisha yangu, na ni kwa kiasi gani nilivyo mpumbavu kukata tamaa juu yako na kuzitupa kumbukumbu zote nzuri tulizoshea pamoja.
Wakakumbatiana kwa upendo na mapenzi yao yakachanua upya, wakaandika tena lile tukio la kuwaunganisha pamoja na kwenda kuweka pesa benki.
Na notebook wakaitunza tena katika sehemu iliyo salama kwa ajili ya kuendelea kuandika rekodi.
_______________________________________
Ndoa sio mchezo wa kuigiza, sio kitu rahisi ila ni nzuri. Mtabishana, Mtagombana na kununiana ila ni kawaida kwa sababu kila mmoja ametoka katika familia zenye historia tofauti.
Usitegemee kila utakachozungumza kitakubaliwa na mwenzako moja kwa moja bila kutoa maoni yake. Ila kabla ya kukata tamaa katika ndoa fikiria nyakati nzuri kabisa mlizoshea pamoja na kuwaweka karibu.
Kuvumiliana na kujaribu kurekebisha madhaifu ya kila mmoja wetu hufanya ndoa kuwa na afya na huwaweka nyote wawili karibu zaidi.
UVUMILIVU + SALA + MSAMAHA + HESHIMA = NDOA IMARA.
TAKE CARE, BECAUSE I CARE!
UKIIPENDA TAG NA SHARE TAFADHALI ILI WENGINE WAPATE UJUMBE HUU

UPENDO WA MAMA



Alikuwepo mama mmoja aliyekuwa chongo na mwanae alimchukia kwa sababu ya kuwa chongo. Mwanae alijisikia aibu kutembea na mama yake mwenye jicho moja na hakupenda watu wajue kuwa yule ni mama yake.
Hata alipokuwa shuleni hakupenda mama yake amtembelee, na ikitokea mama yake akamtembelea basi watoto wenzie watamcheka siku nzima na kumtania. Hii ilimfanya mtoto huyu kujisikia vibaya sana na wakati mwingine kujuta kuwa na mama wa aina hiyo.
Lakini mama alimpenda mwanae na hakuonesha kukasirika hata pale mwanae alipomnyanyapaa waziwazi.
Badae mtoto akakuwa akamaliza masomo yake na kupata kazi nzuri. Akafurahi kuwa sasa amepata kazi atakuwa mbali na mama yake 'chongo' anayemtia aibu.
Akachagua kufanya kazi mji wa mbali na alipo mama yake. Akafanikiwa kazini kwa kupandishwa cheo na akawa mtu mashuhuri mwenye mali na mwenye heshima kubwa ktk jamii yake.
Siku moja asubuhi akasikia wanae wakilia walipokua nje wakicheza.. Alipowauliza wakasema kuna mtu anawatisha.. Akatoka nje kujua nani anayewatisha wanae. Kufika akamkuta mwanamke mmoja mzee mwenye jicho moja (chongo). Kumbe wale watoto walitishwa na chongo la yule bibi.
Alipomtizama vizuri yule mwanamke akamgundua ni mama yake mzazi. Alikua amechoka na amezeeka sana. Amedhoofu mwili na anaonekana mgonjwa..
Mtoto kwa hasira akamuuliza "mama umekuja kufanya nini hapa? Kama una shida ungenipigia simu sio kuja? kwanza nani kakuonyesha ninapoishi? Na nani kamruhusu mlinzi kukufungulia mlango? Ona sasa umewatisha wanangu kwa chongo lako"
Mama yake akasema "samahani mwanangu, sikujua naomba unisamehe". Kisha mtoto akamchukua mama yake akamtoa nje na kumpeleka kituo cha basi ili arudi kijijini.
Baada ya siku chache kupita, yule jamaa akapata taarifa kuwa mama yake ni mgonjwa sana na anahitaji kumuona. Akaondoka kwa siri kwenda kijijini ili akasikie mama yake anataka kumwambia nini.
Alipofika akakuta watu wengi wamekusanyika nyumbani kwao. Alipouliza akaambiwa mama yake alifariki baada ya kuugua sana bila msaada wowote.
Alipoingia ndani akakuta barua aliyoandika mama yake.. Barua ilisomeka hivi...
"Kwako mwanangu mpendwa wa pekee,
Naandika barua hii nikiwa kwenye maumivu makali sana na sijui kama nitapona.. Nimeugua nikakosa matibabu kwa kutokuwa na fedha. Sikuwa na mtu mwingine wa kumueleza shida yangu zaidi yako wewe mwanangu wa pekee... Lakini nilipojitahidi kuja kwako angalau unisaidie matibabu ulinifukuza na kudai nawatisha wanao kwa chongo langu ! Uliniumiza sana mwanangu sitisahau maishani mwangu ila nimekusamehe.
Baba yako alifariki ukiwa mdogo sana. Nami sikubahatika kupata mtoto mwingine. Nilikulea kwa nguvu zangu zote na umasikini niliokuwa nao ilikuwa nikitegemea badae utanisaidia lakini umenitelekeza na kunitupa kwa sababu tu mimi mama yako ni chongo ! Hivyo unaona aibu kuwa nami....
Nisamehe kwa kuwatisha wanao kwa chongo langu, nisamehe kwa kuja kwako bila ya taarifa, nisamehe kwa kukufanya uchekwe na wenzio kwa kuwa mimi mama yako ni chongo....
Lakini naomba nikupe siri ambayo hukua unaijua ewe mwanangu, wewe ndiye uliyezaliwa ukiwa chongo. Ulikua na jicho moja tu. Nikaumia sana kuona mwanangu ana jicho moja, atawezaje kuishi na kukabiliana na changamoto za maisha.. Nikaomba madaktari wanitoe jicho langu moja wakupe wewe, Niliona ni heri mimi niwe chongo kwa kuwa nimeshaona mengi sana duniani kuliko wewe..
Na ulipowekewa jicho langu nilifurahi kukuona una macho mawili nikajua utaweza kuzikabili vema changamoto za dunia hii... Na hakika jicho langu limekusaidia kwani wewe ni mtu mashuhuri na tajiri sana kwa sasa...
Lakini kwa jinsi ninavyoumwa najua nitakufa. Ila nafurahi kuwa nakufa nikiwa nimetimiza haja ya moyo wangu. Kwa kutumia jicho langu umeweza kuwa msomi mzuri na tajiri unayeheshimika na jamii yote.. Wasalimie wajukuu zangu na waambie wawe na amani hawataniona tena nikienda kuwatisha na chongo langu.. Please take care of my eye...
Akupendaye,
Mama"
Alipomaliza kuisoma barua hii akalia sana. Akatamani mama yake afufuke amuombe msamaha na amlipe kwa wema wake aliomtendea.. Lakini haikuwezekana, it was TOO LATE.!
MORAL OF THE STORY.!
Nyuma mafanikio ya kila mwanaume yupo mwanamke. Anaweza kuwa mama yako, mke wako, dada yako au mchumba wako.. Je unatambua nafasi yake katika mafanikio yako au unampuuza tu?
Wapo wanawake ambao walijitoa sadaka ili uweze kuwa hapo ulipo. Jiulize mama yako amefanya mangapi kukufikisha hapo.
Hadithi hapo juu inatueleza juu ya mama aliyetoa jicho lake kwa mwanae.. lakini jicho ni kielelezo tu cha yale wanayofanya mama zetu.
Kuna wengine jicho lao ni vibarua alivyokua anafanya ili wewe usome.. Pengine jicho lake ni namna alivyokua akijinyima kwa kuvaa nguo moja mwaka mzima ili upate ada ya shule na mahitaji mengine.. Je umewahi kumshukuru mama yako kwa kutoa jicho lake kwa ajili yako??
Mpende sana mama yako.. Wapende wanawake wote, waheshimu, walinde, wajali. Wanapitia magumu mengi sana ili kutufanya sisi wanaume tuwe kama tulivyo.
Share ujumbe huu kama sehemu ya kuonesha kutambua mchango wa wanawake katika jamii uliyopo.






KISA.
Kulikua na mtu mmoja anamlea mama yake na mkewe, na alikua anafanya kazi ya utumishi kwa bosi mmoja, na alikua anatimiza majukumu ya kazi yake vizuri.
Siku moja hakuweza kufika kazini, bosi wake akasema katika nafsi yake lazima nimuongezee mshahara hata isitokee siku kutofika kazini, na kwa hakika hatoacha kuja kwa matumaini ya kuongezewa mshahara,
Pindi alipokuja siku ya pili yake akampa mshahara wake na akamuongezea kama alivyoahidi, lakini yule mfanyakazi hakuzungumza chochote na wala hakumuuliza bosi wake...sababu ya kumuongezea mshahara.
Na baada ya muda yule mtumishi hakutokea kazini kwa mara nyengine, bosi akakasirika sana na akasema;" nitampunguzia mshahara niliomuongezea,alipokuja kazini akampunguzia mshahara.
lakini yule mfanyakazi hakusema chochote na wala hakumuuliza bosi wake.. sababu ya kumpunguzia mshahara.
Bosi wake akashangazwa sana kwa kitendo kile,kisha akasema kumwambia; nilikuongezea mshahara hukusema chochote ,na nimekupunguzia hukusema chochote, yule mfanyakazi akasema; siku ya kwanza ambayo sikutokea kazini mwenyezi mungu alijaalia mtoto, na kwa ajili hio ndio maana sikutokea kazini, basi uliponiongezea mshahara nikasema hii ni riziki ya mtoto wangu amekuja nayo.
Na niliposhindwa kuja mara ya pili Mama yangu alikua amefariki, na wakati uliponipunguzia mshahara nikasema hii ni riziki yake ameondoka nayo.
Uzuri ulioje kwa mtu kutosheka na kuridhia kile ambacho mwenyezi mungu amempa, na kuamini kwamba riziki inatoka kwa M/mungu

UNGEFANYA NINI?



Mwanamke alimkimbia mumewe na akamuachia mtoto mwenye miaka mitatu.
Sababu kubwa ya kumkimbia mumewe ni kwamba alipata boyfriend mwenye hela ambaye alikuwa akiishi Michigan huko Marekani.
Huyo Boyfriend au mchepuko wake walijuana kupitia mitandao ya kijamii. Walizoeana sana na mwisho yule boyfriend wake akamuahidi kumtafutia viza ya kuishi Marekani.
Na kweli baada ya miezi kadhaa yule mwanamke alimtoroka mumewe na kutokomea Marekani, huku akiacha taarifa kwamba asitafutwe tena, anaenda kuanza maisha mengine mapya. (mumewe alifirisiwa kutokana na kutuhumiwa ubadhirifu wa mali za kampuni alikokuwa akifanya kazi).
Kutokana na msongo wa mawazo na upweke kwa kipindi kirefu tokea mkewe amtoroke, yule mwanaume akaamua kuoa mke mwingine.
Kwa bahati mbaya yule mwanamke mwingine aliyeolewa hakuweza kushika mimba. Hata hivyo yule mwanamke mwingine alimtunza vema mtoto wake wa kambo kama mwanae vile.
Miaka michache baadae, yule mume alifariki kwa ajali ya gari alilokuwa akisafiri nalo kwenda kijijini kufanya biashara ya mazao.
Mke wake wa pili alifanya kila jitihada kwa uwezo wale wote kumsomesha yule mtoto, na Mungu hakunyimi vyote kwani yule mtoto alikuwa na uwezo mkubwa wa kiakili.
Mwanamke aliuza nyanya sokoni, alitembeza ndizi, alichoma mahindi barabarani na kadharika ilimradi aweze kujitunza yeye na yule mtoto wake wa kufikia.
Yule mtoto alijua kwamba yule ndiye mama yake halisi na ndiye aliyekuwa akimuita mama.
Mama yake halisi aliyetorokea Michigani, Marekani, hakuwahi hata siku moja kutuma salamu au kuwasiliana na mtoto wake, ingawa alipata habari kwamba mumewe wa zamani alifariki kwa ajali.
Miaka mingi ilisonga na kijana alikuwa kwa akili na kimo, alikuwa Chuo kikuu akisomea Uhandisi wa mafuta na gesi (Bachelor of science in petroleum Engineering).
Mama yake halisi aliyeko Marekani hakuweza kupata mtoto tena na yule mwanaume mwingine aliyemuoa, na kwa hilo yule mume wake mpya aliamua kumtimulia mbali.
Kwa kutambua kuwa alifanya kosa kumkimbia mwanae, aliamua kurudi nyumbani kumtafuta mwanae na kumkabidhi utajiri alioupata akiwa Marekani (gawiwo la nusu kwa nusu la mali baada ya kutalikiana na mumewe wa Marekani)
Bahati mbaya alifika na kumkuta mwane akipigania kati ya uhai na kifo kutokana na kufeli kwa figo zake. Madaktari walikuwa wakihitaji pesa nyingi kwa ajili ya upasuaji, pesa ambazo mama yake wa kambo alishindwa kabisa kuzipata.
Mama yake halisi kutoka Marekani aliingilia hilo suala na kulipa pesa zote za hospitali kwa ajili ya matibabu, pia akatoa figo yake moja na maisha ya kijana yakawa yameokolewa.
Baada ya matokeo ya mwisho ya chuo kikuu kutoka, kijana alipata ufaulu wa hali ya juu (first class degree) na akapewa ufadhili wa kwenda kusomea shahada ya uzamivu (masters) na baada ya hapo udaktari wa falsafa (phd) huko Burnley, Uingereza.
Katika kupokea cheti chake siku ya mahafali chuoni kwao, makamu mkuu wa chuo alimpa kipaza sauti kijana na kumwambia amuite mama yake katika stage na kupokea cheti cha heshima.
Baada ya makamu mkuu wa chuo kusema hayo, mama yake halisi aliyemkimbia alisimama na kujiweka sawa kusubiri kuitwa na mwanae, wakati mama yake wa kambo aliyemlea tokea mdogo akiwa bado amekaa huku machozi mengi yakimtoka huku akimuangalia mwanae wa kufikia kule mbele.
Jibu naliacha hewani.........................
Fikiria wewe ndio huyo mtoto, utamuita nani aje kule stejini kupokea hicho cheti?
A) Mama wa kambo
B) Mama mzazi
Nahitaji majibu yenu, kama huna share kwa wengine waje na majibu.

Nimeona ni vema ku share na nyinyi story hii inayo gusa moyo, hasa kwa wewe uliye Mkristo.
Mchungaji mmoja alijibadili na kuwa omba omba katika viunga vya kanisa alilokuwa akitarajia kutangazwa jumapili hiyo kama ni mchungaji mpya wa kanisa lile akitokea mji mwingine.
Alitembea kuzunguka lile kanisa akiwa amevaa nguo kukuuu zilizochanika chanika huku akipishana na watu waliokuwa wakiingia kanisani. Ni watu watatu tu ndio waliomsalimia.
Wengine wote hawakutaka hata kumuangalia mara mbili, walipitiliza moja kwa moja na kuingia kanisani.


Aliwaomba watu msaada wa chakula au hela ya kula hakuna hata mmoja aliyempa chochote.
Akaenda katika malango ya kanisa na kukaa katika ngazi akaweka chombo chake ili aguswae atoe msaada lakini hakuna hata mmoja alietoa hata senti moja.
Akainuka na kwenda mbele kabisa ya kanisa, akakaa benchi la kwanza kabisa, mzee wa kanisa akamwambia aondoke pale na akakae nyuma kwa vile ile sehemu ni ya watu maarafu (VIP).
Akaenda nyuma ya kanisa na akakaa benchi la mwisho kabisa lilikowa halina watu, maana wote walionekana kulikwepa. Akiwa amekaa akawa anasikiliza matangazo ya wiki kutoka kwa mzee wa kanisa.


Akasikiliza wageni wapya wakitajwa na kukaribishwa katika kanisa ila hakuna hata mmoja aliyemkaribisha kwa kuwa nae alikuwa mgeni mazingira yale.
Akaendelea kuwatizama watu waliokuwa wakimuangalia na kutoa mshangao ambao ulikuwa na tafsiri kwamba hatakiwi mahala pale.

Baadae kiongozi wa kanisa akaenda pale mbele kutangaza jambo la muhimu. Akasema kwamba anayo furaha kumtambulisha mchungaji mpya mbele ya waumini wote.
Waumini wakasimama na kutizama huku na huku wakiwa wanapiga makofi. Yule ombaomba akasimaa kutokea kule nyuma na kuanza kutembea kuelekea mbele ya aisle.

Kufikia hapo watu wakaacha kupiga makofi na kanisa likawa kimya wote wakimtizama yeye...akatembea mpaka madhabahuni na kuchukua kipaza sauti. Akasimama pale kwa dakika kadhaa, akakohoa kidogo na kunukuu mistari kutoka kitabu kitakatifu cha Mathayo 25:34-40 akaanza
"Kisha mfalme atawaambia wale walio mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu; kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha; nalikuwa uchi, mkanivika, nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitizama, nalikuwa kifungoni mkanijia...Ndipo wenye haki watakapomjibu wakisema, Bwana ni lini tulikuona una njaa, tukakulisha au una kiu, tukakunywesha? Tena ni lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha? Au u uchi tukakuvika? Ni lini tena tulipokuona u mgonjwa au kifungoni tukakujia?

Na mfalme atajibu, akiwaambia, AMIN AMIN NAWAAMBIA. KADIRI MLIVYOMTENDEA MMOJAWAPO WA HAO NDUGU ZANGU WALIO WADOGO, MLINITENDEA MIMI"
Baada ya kunukuu hayo, kwa masikitiko na uchungu mwingi moyoni mwake akajitambulisha mbele yao kwamba yeye ndiye mchungaji mpya wa kanisa lile na kuwaeleza ni nini amejifunza kutoka kwao asubuhi ile.
Wengi wakaanza kulia huku wameinamisha vichwa vyao chini.


Akawaambia "Leo naona ni mkusanyiko wa watu, ila sioni kanisa la Mungu. Dunia inayo watu wengi wa namna yenu, tunaleta mazoea hata kwenye ibada sasa, kimsingi Mungu tunaemuabudu hayupo mioyoni mwetu. Wakristo mnatakiwa muwe wanafunzi wa Yesu kristo wa kufuata mafundisho na kutenda mema kama yeye alivyofanya. Lini mtaamua kuwa wanafunzi wa Yesu!?
Baada ya kusema hayo akaahirisha ibada mpaka jumapili inayofuata baada ya kutimiza neno la Mungu kupitia vitendo.


___________________________________________
Basi wewe uliye mkristo, zitafakari njia zako, kwenda kanisani kila Jumapili haitoshi, tuishi katika misingi ya kweli ya ukristo huku tukiwa na moyo wa kuwasaidia wale wote wasiojiweza.
Mwenyezi Mungu atubariki, tuishi vema sawasawa na vile yeye apendavyo.
Kwanini tusiseme 'Amen'.

MKRdezign

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget